
CROSAT yashiriki Marathoni ya maadhimisho ya miaka 10 TARI
August 8, 2026
The 2nd CROSAT Biennial Scientific Conference
October 1, 2026Chama cha Sayansi ya Kilimo Mazao (CROSAT) kimewasisitiza vijana wabunifu katika sekta ya kilimo umuhimu wa kuwa na washauri sahihi wenye uzoefu na uelewa wa sekta ili kuwasaidia kuendeleza mawazo yao ya kibunifu, kuyabadilisha kuwa suluhisho zinazotekelezeka na hatimaye kuyafikisha katika soko.
Ujumbe huo umetolewa wakati CROSAT iliposhiriki katika mdahalo wa vijana ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), uliowakutanisha vijana wabunifu pamoja na wadau mbalimbali wanaochangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini. Miongoni mwa wadau walioshiriki ni kutoka katika Taasisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Benki ya Maendeleo (NMB), Kampun8 ya pembejeo za kilimo ya FarmBase, Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), pamoja na wadau wengine.
Katika mdahalo huo, CROSAT iliwakilishwa na Bi. Jenipher C. Tairo, Katibu Msaidizi wa Uhamasishaji wa CROSAT, ambaye aliwapongeza vijana kwa ubunifu, uthubutu na jitihada zao katika kutafuta suluhisho za changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo. Alieleza kuwa mawazo mazuri ya kibunifu yana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa pale wabunifu wanapopata mwongozo kutoka kwa washauri wenye uzoefu, maarifa ya kitaalamu na mitandao sahihi ndani ya sekta husika.
Bi. Tairo alisisitiza kuwa kuwa na mshauri au washauri sahihi kunaweza kumsaidia kijana mbunifu kuboresha wazo lake, kutambua mahitaji halisi ya wakulima na soko, kujenga mtandao wa wadau, pamoja na kuelewa njia mbalimbali za kuendeleza na kufikisha ubunifu kwa watumiaji. Alibainisha pia kuwa ushauri endelevu unaweza kuwasaidia vijana kuepuka baadhi ya changamoto zinazoweza kuchelewesha maendeleo ya ubunifu wao na kuwaunganisha na fursa za ushirikiano, utaalamu na masoko.
Sambamba na hilo, Bi. Tairo aliwakaribisha vijana wabunifu kujiunga na CROSAT ili kupata fursa ya kuunganishwa na watafiti, wataalamu, taasisi na wadau wengine katika sekta ya kilimo. Kupitia mtandao huo, vijana wanaweza kupata mazingira bora ya kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kupata mwongozo unaoweza kusaidia kuendeleza bunifu zao kutoka hatua ya wazo hadi kuwa teknolojia, bidhaa au huduma yenye manufaa kwa wakulima na jamii kwa ujumla.
Mdahalo huo ulihudhuriwa na takribani vijana wabunifu 88 kutoka maeneo mbalimbali, na Taasisi za elimu ya Juu kama vyuo vikuu vya Mzumbe, Ardhi, UDSM, pamoja na vijana wanaoatamiwa kwenye mradi wa BBT ambao walipata fursa ya kuwasilisha mawazo na ubunifu wao, kujifunza kutoka kwa wataalamu na wadau wa sekta ya kilimo, pamoja na kujenga mitandao itakayowawezesha kuendeleza suluhisho zao.
CROSAT itaendelea kushirikiana na COSTECH pamoja na taasisi na wadau wengine katika kujenga mazingira yanayowawezesha vijana kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kutatua changamoto halisi zinazokabili sekta ya kilimo. Ushirikiano huo ni muhimu katika kukuza kizazi kipya cha watafiti, wabunifu na wajasiriamali wenye uwezo wa kuchangia katika kuongeza tija, kuimarisha mnyororo wa thamani, kuongeza ushindani wa sekta ya kilimo na kuchochea maendeleo endelevu ya kilimo nchini Tanzania katika kufikia shabaha za DIRA 2050.







